Sunday, March 21, 2010
ULINZI WAIMARISHWA FUKWE ZA AFRIKA KUSINI!!
Moja kati ya papa wala watu ambao wanahofiwa kutishia maisha ya wageni wataoitembelea Afrika kusini wakati wa fainali za kombe la dunia zinazotarajiwa kuanza kutimua vumbi mwezi juni mwaka huu.
Waandaaji wa kombe la dunia huko Afrika Kusini wameimarisha ulinzi na kuongeza doria katika maeneo ya fukwe za bahari kuhofia mashambulizi ya papa wala watu wakati wa fainali za kombe la dunia.
Kwa mujibu wa ofisa mmoja wa usalama katika pwani ya Afrika kusini amesema ulinzi katika maeneo hayo umeimrishwa ikiwemo kuweka nyavu maalum zinazowazuia papa kufika kando ya bahari na hivyo kuwashambulia wageni watakaoitembelea nchi hiyo wakati wa fainali za kombe la dunia.
Naye msemaji wa bodi ya viumbe hao hatari wa baharini Harry Mbambo amesema tayari wameunda timu za waogeleaji waliopatiwa mafunzo maalum ya uokoaji watakaokuwa wakifanya doria za mara kwa mara katika fukwe hizo wakitoa angalizo kuhusiana na viumbe hao.
Amesema kuna matukio mengi ya watu kuliwa na papa katika fukwe za Afrika kusini kwa hivyo ni jukumu lao kuhakikisha wapenzi wa mchezo wa mpira wa miguu watakaoitembelea nchi hiyo wanakuwa salama kwa muda wote wa fainali hizo.
"Tumechukua hatua madhubuti za kuwadhibiti papa ili kuhakikisha kwamba watu watakaokuja kuogelea katika fukwe hizo wanakuwa salama muda wote."
Idadi kubwa ya watu wamekuwa wakishambuliwa na papa wala watu kila mwaka katika fukwe za nchini humo.
Idadi kubwa ya matukio ya watu kushambuliwa na papa wala watu yameripotiwa katika maeneo ya Durban,mji ambao unaopatikana katika jimbo la KwaZulu-Natal.
Msemaji huyo ameongeza kuwa baadhi ya nyavu hizo maalumu zimewekwa toka mwaka 1960 ambapo toka kuwekwa kwake zimepunguza idadi ya mashambulio ya papa wala watu dhidi ya binadamu.
Akizungumzia doria hizo amesema zitahusisha ukaguzi wa nyavu kama ziko salama pamoja na kutoa tahadhari kwa watu walio katika fukwe husika pale dalili za kuwepo viumbe hao zinapojitokeza.
Zaidi ya wageni wapatao 450,000 wanatarajiwa kuitembelea nchi hiyo wakati wa fainali za kombe la dunia zitakazo anza kutimua vumbi lake mapema Juni 11 mwaka huu.
Wengi wa wageni hao wanategewa kutembelea fukwe za nchi hiyo ikiwemo ile fukwe ya Durban,ambayo itakuwa na hali hewa ya jotom kiasi licha kwamba fainali hizo zinafanyika wakati nchi hiyo ikiwa katika majira ya baridi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Hao watu wanaenda kutazama mpira au kuogelea baharini :-)
ReplyDelete